2 Wakorintho 5:7
"(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.)"
Tunapozungumzia imani mara nyingi watu hufikiri tu juu ya imani ya kutenda miujiza ,au kuponya wagonjwa .
Lakini nivugumu kujua kwamba Ukristo mzima ni imani .

IMANI YA MKRISTO NINI?
(Yohana 3:16)
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele"
(Waefeso 2:8-9)
"Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu".

Kwanza imani ya Mkristo ni kuamini kwamba Bwana Yesu amekufa msalabani kwa ajiri ya dhambi za watu wote , mtu akitubu kwa dhati kwa kufanya damu ya Bwana Yesu kuwa dhabihu ya dhambi zake ,Mungu anamsamehe dhambi na kumbatiza kwa Roho Mtakatifu, Mtu aliyetubu dhambi kwa damu ya Bwana Yesu hana hukumu ya dhambi tena ,anahesabiwa haki bure , anahesabiwa haki ya kuwa mrithi wa ahadi zote za Mungu kama vile kupata uzima wa milele, kulindwa, kupata baraka ,kusema na Mungu nk.

Mtu anapata haki zote kwasababu ni mwana wa Mungu. Siyo mtumwa tena ni mwana wa Mungu . Huyu mtu anatakiwa awe na imani hiyo kwamba mimi ni mwana wa Mungu nimezaliwa katika Roho kwa ubatizo na ni mrithi wa ahadi zote za Mungu na jambo hili limefanyika kwa Neema ya Mungu siyo kwa juhudi za mtu, yaani siyo kwa Sheria au mapenzi ya Mtu ni zawadi ya Mungu.

Mtu ambaye ni mwana wa Mungu anadhihilisha tunda la Roho Mtakatifu na karama za Roho Mtakatifu . Mtu huyu ambaye ni mwana wa Mungu imani yake huonekana katika hayo, pia imani yake huonekana katika Kumuabudu Mungu , kuomba ,kumtumikia Mungu kwa mali zake alizobarikiwa na Mungu.pia kushirikiana na wenzake katika kushuhudia Neno.
Mtu ambaye ni mwana wa Mungu anauhakika kwamba yeye ni mrithi wa uzima wa milele na ahadi zote za Mungu . Mtu huyu ni mwenye haki wa Mungu.
Mtu ambaye ni mwana wa Mungu hafuati tamaa za mwili ila anamfuta Roho Mtakatifu .
Huko ndiyo kuenenda kwa imani.

KUISHI KWA MAPENZI YA MUNGU.
Lakini jambo lingine Mkristo huishi kwa Mapenzi ya Mungu, huyafanya yale ambayo Roho Mtakatifu humuongoza kuyafanya. Mkristo anamtii Roho Mtakatifu . Roho Mtakatifu anataka tuwe na Upendo maana upendo ndiyo utimilifu wa Sheria. Upendo kwa Mungu na Upendo kwa watu. Lakini Mkristo anatakiwa azidi kumuomba Mungu ili matunda ya Roho mtakatifu yazidi kuonekana . (Wagalatia 5:22-23)
[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
[23]upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria."
Pia mkristo anatakiwa amshuhudie Bwana Yesu kwa mali zake ,kwa akiri zake na kwa nguvu zake zote.
(Mathayo 28:19)
"Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu"

IMANI YA WOKOVU.
Lazima mkristo anatakiwa kuamini kwamba amekwisha kushinda Dunia. Lazima ajitambue kwamba ameokoka . Lazima ajitambue kwamba yeye ndiye mwenye kiti Mbinguni. Nasema hili kwasababu kuna watu wanajiita wakristo lakini bado siyo wakristo wanatumikishwa na tamaa za dunia , wapo kwenye mikono ya shetani wakitenda kila uovu huku wakisingiza kwamba tutaokolewa kwa neema.
Ndungu yangu Biblia inasema tumeokolewa siyo tutaokolewa, Imani ya mkristo ni kuamini kwamba Bwana Yesu ameniokoa na mimi ni Mrithi wa uzima wa milele , sio kusema ataniokoa hatuna imani hii. Ni lazima uamini kwamba wewe ni mshindi wa hii Dunia kwakuwa ndani yako yuko Mkuu kuliko Shetani.
(1 Yohana 5:4-5)
[4]Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.
[5]Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?

Mkristo ni mwana wa Mungu, hana imani ya kushindwa anaimani ya kushinda. Hiyo ndiyo imani inayompendeza Mungu. Mkristo amekombolewa tayari, ameokoka tayari. Hiyo ndiyo Imani ambayo Mungu anasema mwenye haki wangu ataishi kwa Imani.

IMANI POTOFU.
Zipo imani potofu zilizozuka katika makanisa nakuitwa imani lakini siyo imani ya mkristo. Kwamfano imani na Matendo ya Sheria.

Matendo ya sheria hayampi mtu haki ya kuitwa mwana wa Mungu na hayampi mtu haki ya kupata uzima wa milele .Ndiyo maana tunasema Torati haimpi mtu haki yakupata uzima wa milele . Torati ni sheria siyo imani mtu akitenda yaliyo katika Torati anatakiwa kupata malipo , lakini uzima wa milele siyo malipo ni Neema ya Mungu. Haki ya kupata uzima wa milele inatolewa kwa Neema ya Mungu . Haki ya kupata uzima wa milele ni bure kabisa tumeipata kwa Neema .
(Wagalatia 3:10-12)
"Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.
Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.
Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo."

Nasema hili kwasababu wapo watu wanawatengenezea wakristo imani potofu na kuwaambia hiyo ni imani ya kikristo. Wapo watu wanasema usipotoa malimbuko hubarikiwi , usiposhika sabato huendi Mbinguni, usipotoa fungu la kumi hupati ulinzi , usipojiepusha na vyakula najisi huendi Mbinguni. Hiyo siyo imani ya kikiristo hiyo ni imani nyingine na Injili nyingine.
Imani ya mkristo ni kuzaliwa kuwa mwana wa Mungu na kuishi maisha matakatifu kama mwana wa Mungu , haki zote anazipata bure kabisa ,haki zote anazipata kwa kuwa ni mwana wa Mungu.

Watu wengi huchanganya maandiko na kuyatafsiri vibaya na kuwatia watu katika Torati moja ya maandoko yanayo tafsiriwa vibaya ni haya:-(Yakobo 2:17-18)
[17]Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.
[18]Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu."

Basi wapo watu hutumia andiko hilo kama kigezo cha kuwatia watu katika Torati ,bila kuelewa matendo yanayotajwa hapo ni matendo ya namna gani? Matendo yanayotajwa hapo ni matunda ya Roho Mtakatifu .
(Wagalatia 5:22-23)
[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
[23]upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria."
Hayo ndiyo matendo ambayo Yakobo anasema , Yakobo hazungumzii kushika Torati . Ndiyo maana anazungumzia rehema ukisoma:-
(Yakobo 2:15-16)
"Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki,
na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?"

Umeona anachosema Yakobo hapo hiyo siyo Torati ni tunda la Roho Mtakatifu siyo Torati.
Kwahiyo matendo ambayo yanatakiwa yaonekane kwa mkristo ni matunda ya Roho Mtakatifu siyo kushika Torati.
Unakuta mtu anajisifu kanisani mimi fungu la kumi sijawahi kuacha kutoa ,mtu anadiriki kusema katika fungu la kumi Mungu hanipati kabisa. Lakini mtu huyo hana Matunda ya Roho Mtakatifu haonyeshi Rehema kwa wahitaji ,hana Upendo ,hana fadhili ila anajisifia kushika Torati akifikiri kwamba kwakufanya hivyo ndiyo anampendeza Mungu kumbe anatumikia Agano la laana na kuacha Agano jipya la Neema.

Matokeo yake sasa unakuta mtu anaenda kwa mchungaji kumhoji mbona mimi natoa fungu la kumi kwa uaminifu lakini kuku wangu wamekufa? Mchungaji naye anamtungia uongo mwingine anamuambia kwasababu huji kanisani jumatano na ijumaa na kwa wiki hufungi mara mbili. Hivyo ndiyo wanatengenezewa imani potofu. Wanafikiri hayo matendo waliyojitungia wenyewe ndiyo yanawapa haki yakulindwa na Mungu.

Haki ya kulindwa na Mungu ni bure haipatikani kwa mali au kwa sheria za Torati au za kanisa . Haki ya kulindwa au kubarikiwa au kupata uzima wa milele ikipatikana kwa sheria yoyote haiwi tena neema ila inakuwa ni malipo. Imani ya mkristo siyo kulipwa na Mungu , imani ya Mkristo ni kuzaliwa kuwa mwana wa Mungu na kupata haki zote kama mwana wa Mungu .
( Warumi 4:3-6,13-14)
"[3]Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.
[4]Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
[5]Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
[6]Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,"

Umeona maandiko yanavyosema kwamba mtu akitaka kuhesabiwa haki kwa sheria inakuwa siyo Neema ila ni malipo. Na huyo mtu atakuwa amejitoa katika imani ya mkristo maana imani ya mkristo kila kitu hufanyika kwa Neema iliyopo ndani ya kristo Bwana Yesu. Mungu anapenda mtu anayeishi kwa imani tena imani sahihi siyo imani yakutengeneza . Maana kuna watu wanajitengenezea imani , unakuta mtu anaambiwa inenee hiyo sadaka yako. Au unasikia toa sadaka nono nono kisha inenee , sema kitu unashotaka kwenye hiyo sadaka. Hiyo ni imani ya kishirikina Mungu hajibu maombi eti kwasababu tumetoa sadaka nono, wala Mungu hajibu maombi kwasababu tumetoa sadaka. Mambo ya kunenea sadaka siyo imani ya Mkristo. Mungu hutupa kila kitu kwasababu ni Mungu mwenye Upendo na Neema na Rehema siyo kwasababu tumetoa sadaka nono. Ukiwa mwana wa Mungu kila kitu ulichonacho ni cha Mungu , na ahadi zote za Mungu ni zako. Huna haja yakufikiri kwamba Mungu anafanya biashara na watu ,kwamba ete watoe ndiyo Mungu atende.

Unapokuwa mwana wa Mungu ,siyo kwamba wewe ni mwana wa kuitwa tu ni mwana kabisa . Kwahiyo unapofanya kazi za Baba yako usitegemee malipo kwasababu kazi zote ni za kwako .Upo ndani ya Ufalme wa Baba yako, upo ndani ya nyumba ya Baba yako , sasa unataka ulipwe nini ikiwa kila kitu ni chako na kila ulisho nacho ni cha Mungu ambaye ni Baba.
(Warumi 4:13-14)
"Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.
Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika."

Umeona kama tunarithi kwa sheria inamaana hiyo siyo imani , wala siyo ahadi tena pia hatutakuwa wana wa Mungu ila tutakuwa watumwa ambao tunasubiri kulipwa kwa jinsi tulivyofanikiwa kushika Sheria. Je kuna mtu anaweza kusimama mbele za Mungu na kusema Mungu nilipe haki ya kupata uzima wa milele maana nimetimiza Sheria? Hakuna hata mmoja . Sasa kama hakuna kwanini leo hii wakristo mnajitia katika imani potofu ya kudai ulinzi wa Mungu kwa kutimiza kutoa fungu la kumi? Kwanini mnadai baraka kwa kutoa malimbuko? Kwanini mnadai haki ya kupata uzima wa milele kwa kushika sabato? Kwanini mnatoa sadaka za ukombozi wa mali ,na watoto ? Kwanini mnatoa sadaka za kuweka watoto wakfu? Kwanini kuita vyakula najisi mnataka Mungu awahesabie haki kwa kutokula chakula najisi?

Haki za Mungu ni Neema kwa watoto wake tumepata zote kwa kuzaliwa kuwa wana wa Mungu. Hiyo ndiyo Imani ya mkristo .Lazima aamini hilo kwamba amezaliwa kwa neema ya Mungu kwa kuwa mwana wa Mungu na ni mrithi wa ahadi zote za Mungu kwakuwa ni mwana wa Mungu.
Imani ya kwanza ya mkristo ni hiyo kwamba mimi ni mwana wa Mungu ni mrithi wa ahadi zote za Baba na ninaishi kwa matunda ya Roho Mtakatifu aliyeko ndani mwangu.

IMANI ILIYOKUFA.

ipo imani iliyokufa , kuna wakristo wanasema tuna mwamini Mungu, tuna amini katika jina la Bwana Yesu ,lakini maisha yao hayana matendo yanayodhihilisha imani yao. Tumeona kwamba tunda la Roho Mtakatifu linatakiwa lionekane kama matendo yanayodhihilisha imani yao . Huwezi ukasema mimi na mwamini Bwana Yesu lakini unaishi katika utumwa wa dhambi unakuwa na imani iliyokufa . Pia wapo watu katika makanisa wanaimani iliyokufa , wanajiita tu tumeokoka lakini matendo yao yanayodhihilisha wokovu hatuyaoni.

Unakuta Mchungaji anahubiri upendo lakini yeye hana upendo. Kanisa linakaa mwaka mzima huoni matendo ya Rehema ,lakini wanasema tumeokoka tuna Roho Mtakatifu .
Kama Roho Mtakatifu hadhihiliki katika kanisa katika matunda na karama ,hilo kanisa linaimani iliyokufa.
(Yakobo 2:26)
"Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa."
Ukisema tu kwamba wewe ni mkristo lakini hatukuoni ukifanya ibada ,hatukuoni ukimuomba Mungu hatukuoni ukishirikiana na wenzako katika kushuhudia neno, hatukuoni ukimtumikia Mungu Katika mali alizokupa , wala hutuoni matunda ya Roho Mtakatifu ndani mwako , Hapo tunasema wewe unaimani iliyokufa.
Usikubari sasa kuwa na imani iliyokufa maisha yote ya mkristo ni imani na imani hii inadhihilishwa kwa kutumikia karama ile Mungu aliyokupa na vipawa Mungu alivyokupa na kuonyesha tunda la roho Mtakatifu. Hayo ndoyo matendo ya imani ya mkristo siyo kujivunia kushika Torati kama kutahiliwa , kushika sabato na kutokula vyakula nk.

Mungu akubariki.
Www.vop.info.tz
Mwl.Godlisten
0789874316