(Mathayo 5:20)
[20]Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni."

Katika Mlango huu wa 5 wa Injili ya Mathayo Bwana Yesu anaeleza sifa za mtu ambaye yupo ndani ya Ufalme wa Mungu.
Mstari huu wa Ishirini yaana (mathayo 5:20 ) mara nyingi hutumika katika makanisa lakini maana yake hupotoshwa. Unakuta mtu anasema kwenye kanisa kwamba HAKI yenu inatakiwa izidi HAKI ya Mafarisayo halafu anaanza kufafanua matendo ya Torati kwasababu anajua Mafarisayo walikuwa wanashika Torati basi anataka nasisi tushike Torati kwa bidii sana ili tuwashinde HAKI. Huu ni upotoshaji wa Neno la Mungu.

Mafarisayo na waandishi walikuwa wanatafuta Haki mbele za Mungu kwa kushika Torati kama vile walivyotakiwa na Torati wafanye . Kwao ilikuwa sahihi maana ndiyo njia Mungu aliyowapa . Lakini Bwana Yesu katika mathayo 5 anaonyesha udhaifu Mkubwa wakutafuta Haki kwa kutumia sheria . Sheria inawafanya watu kuwa wanafiki. Mafarisayo kwa nje walikuwa wanaonekana wasafi sana kwasababu ya Matendo ya sheria ambayo walikuwa wakiyafanya lakini mioyo yao iko mbali na Mungu.
Utakaso wao ulikuwa ni wa nje tu siyo ndani.Mafarisayo walikuwa wanajivunia kuwa watu safi kwa sababu ya uwezo wao katika kufanya mambo kadhaa kama vile kufunga ,kutoa zaka nk .Kwakutimiza yale ambayo yameandikwa katika Torati walijihesabia Haki . Ona mfano huu ambao ametoa Bwana Yesu.

(Luka 18:9-14)
[9]Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.
[10]Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.
[11]Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
[12]Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.
[13]Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
[14]Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa"

Usafi na utakaso wa namna hii uko chini ya kiwango. Usafi na utakaso wa aina hii unakaza mno mambo ya nje . Kwa Mujibu wa Bwana Yesu usafi na utakaso wa aina hii haiwezekani kumwona Mungu . Watu ambao wametakaswa na kubadilishwa mioyo yao na utakatifu wao ukatokea ndani hao ndiyo watu ambao wapo kwenye Ufalme wa Mungu.

Kwa hiyo Bwana Yesu anaposema Haki yetu inatakiwa izidi haki ya Mafarisayo na waandishi hana maana kwamba tushike Torati sana kuliko wao . Anamaana kwamba utakatifu wetu uanzie ndani katika roho zetu. Kwa hiyo ili mtu awe mtakatifu kutokea ndani lazima azaliwe mara ya pili kwa Roho Mtakatifu ili matendo yake yote yawe ni matunda ya Roho Mtakatifu aliyepo ndani mwake. Hapo ndipo haki yako itazidi Haki ya Mafarisayo .

Unakuta mtu ameona watu wamepunguza kutoa fungu la kumi au hawafungi mara mbili kwa wiki, anaanza kuwatisha kwa kuwasomea hicho kifungu cha Mathayo 5:20 , na kuwatia watu kwenye Torati ibada ambazo siyo zakwetu, ibada za mwili. Huko nikutoelewa Neno la Mungu. Tumuombe Mungu atufunulie maandiko.

Mungu akubariki.
Mwl.Godlisten w Mshigheni
Www.vop.info.tz
0789874316