Utatu Mtakatifu ni fundisho la msingi katika Imani ya Kikristo .
Fundisho la utatu Mtakatifu ni kati ya mafundisho ambayo yameufanya ukristo kuonekana kama Imani yenye utata. Kwa wengine hudhani kwamba utatu mtakatifu ni kuwa na miungu watatu.

1.Je Utatu Mtakatifu nini?
Ni Mungu mmoja kujidhihirisha katika Baba ,Mwana na Roho Mtakatifu.
(1 Yohana 5:8)
"[8]Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja"

Ili tujue ni jinsi gani watatu hawa ni Umoja ,hembu tujiulize.

2. Roho Mtakatifu ni nani?
Roho Mtakatifu ni "ROHO YA MUNGU".

(Mwanzo 1:2) "Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; ROHO YA MUNGU ikatulia juu ya uso wa maji"

Roho Mtakatifu ni ROHO YA MUNGU, Roho ya Mungu iko ndani ya Mungu na ipo kila sehemu ."Roho ya Mungu ni Mungu mwenyewe".
(Zaburi 139:7-8,10)
[7]Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
[8]Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
[10]Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika"

Mungu yupo kila sehemu kupitia Roho wake, Roho ya Mungu ipo ndani ya Mungu na ipo kila sehemu. Roho ya Mungu ni Mungu mwenyewe Kama vile roho ya mtu ni mtu mwenyewe . Huwezi kusema roho ya John siyo John, isipokuwa roho ya mwanadamu haiwezi kuwa kila sehemu na mwanadamu hawezi kutoa sehemu ya roho yake na kuingiza kwa mtu mwingine. Lakini Roho ya Mungu ipo kila sehemu .

Hivyo basi Roho Mtakatifu siyo punzi kama wengine wanavyodhani, wala Roho Mtakatifu siyo nguvu za utendaji kama wengine wanavyodhani. Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe. Kwahiyo tunaposema Roho Mtakatifu ni Mungu ,hatuna maana kwamba ni Mungu tofauti na Mungu kama wengine wanavyodhani.

Sisi tupo ndani ya Mungu kupitia Roho yake pia Mungu yupo ndani yetu kwa sababu Roho yake ipo ndani mwetu. Ndiyo maana tunasema Mungu yupo ndani mwetu na sisi tupo ndani mwake.
(1 Yohana 4:13)
"Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake."

Roho ya Mungu siyo Mungu tofauti na Mungu Baba . Roho ya Mungu ni Mungu Baba mwenyewe.

3. Pia tujiulize, vipi kuhusu mwana?ni nani?

(Yohana 1:1)
"Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu."
Umeona Yohana anavyosema kwamba Neno lilikuwepo tangu mwanzo , lakini hilo Neno lilikuwa ndani ya Mungu , kama Neno lilikuwa ndani ya Mungu maana yake ni Mungu mwenyewe.
(Yohana 1:14)
"Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli."

Umeona hapo tena, Neno ambaye yuko ndani ya Mungu amefanyika mwili na kukaa pamoja na sisi. Asingefanyika mwili tusingemwona maana Neno la Mungu ni Roho. Neno la Mungu ni Roho ya Mungu. Lakini tumemwona Mungu kupitia Neno aliyefanyika mwili ambaye ndiye Bwana wetu Yesu kristo .

Kitendo cha Neno kufanyika mwili hakijabadilisha Uungu wa Neno, bado ni Mungu vile vile , kitendo hicho pia hakijamtoa Neno nje ya Mungu bado Neno yupo ndani ya Mungu vilevile .
(Yohana 14:8-10)
[8]Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.
[9]Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
[10]Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake."

Sasa 'mwana' siyo Mungu tofauti na Mungu Baba maana angekuwa Mungu tofauti asingekuwepo ndani ya Mungu Baba .pia Roho Mtakatifu siyo Mungu tofauti na Mungu Baba maana angekuwa Mungu tofauti asingekuwa ndani ya Mungu Baba.

Kwahiyo Utatu Mtakatifu ni Mungu mmoja kujidhihirisha katika Baba ,Mwana na Roho Mtakatifu. Hivyo katika imani yetu ya Ukristo hatuna miungu watatu ila tuna Mungu mmoja anayejidhihirisha katika Baba ,Mwana na Roho Mtakatifu.