(Matendo ya Mitume 17:23)
"Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua."

Mtume Paulo aliwakuta hawa watu wa Athene wana hekalu ambalo wameandika KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Walikuwa wanafanya ibada kwa huyu Mungu bila wao kumjua , walikuwa wanafanya ibada kwa mungu ambaye hawajui chochote kuhusu yeye. Mtume Paulo alitumia jina hili kama mwanzo wa kuwahubiria watu hawa Injili na kuwafahamisha kuhusu Mungu wa kweli.

Lakini kwa bahati mbaya sana leo hii wapo watu ni wakristo wako makanisani lakini wanamwabudu MUNGU ASIYEJULIKANA.Kwanini nasema hivi? kwasababu wanamwabudu Mungu ambaye hawajui chochote kuhusu yeye.

Sisi wakristo hatupaswi kumwabudu MUNGU ASIYEJULIKANA ,tunatakiwa kuabudu MUNGU ANAYEJULIKANA ambaye amejifunua kwetu kwa kiwango kile ambacho anataka tumjue.
kwasababu Mungu amejifunua kwetu kwa njia mbalimbali .Mungu hachunguziki , yaani akiri za mwanadamu haziwezi kumuelewa Mungu mpaka Mungu mwenyewe atake kujifunua kwa wanadamu . Mungu wetu amejifunua kwetu kwa kiwango kile ambacho amekitaka yeye mwenyewe ili tuweze kumwabudu. Mungu wetu anataka tumfahamu ndiyo maana anasema:-
(Yeremia 9:24)
"bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA,"

Mungu wetu anasema hivi kwamba ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi... Kwahiyo Mtu ambaye anamwabudu Mungu katika Roho na kweli ni yule ambaye anamfahamu Mungu . Hivyo ili ibada yako iwe ya Roho na kweli lazima umfahamu Mungu kwa kiasi kile alichojifunua. Siyo kufahamu mafundisho ya Dini, ni kumfahamu Mungu.maana kuna wengine wanajisifia Shahada za Thiolojia , Thiolojia ni kufahamu Dini ndiyo maana kuna Thiolojia nyingi . Kumfahamu Mungu ni kuwa na mahusiano naye , mahusiano kamili ya Baba na mwana.Ndiyo maana mtu anaweza kuwa na elimu kubwa ya Thiolojia lakini hana Mungu.

Mtume Paulo alikuja kurudia maandiko haya katika wakorintho akisema :-
(1 Wakorintho 1:31)
"kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana"
Angalia hapa mtume Paulo anavyowaambia Waefeso :-
(Waefeso 3:17-19)
"Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo;
ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina;
na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu"

Anawaambia waefeso kwamba wanatakiwa wamfahamu Bwana Yesu na wafahamu upendo wake jinsi ulivyo .Umeona tunatakiwa tumwabudu Mungu tunayemjua . Ili ibada yako iwe katika Roho na Kweli lazima umfahamu Mungu vizuri kwa kiwango kile alichojifunua.

JE TUNA MFAHAMU VIPI MUNGU? Tunamfahamu Mungu kwa jinsi alivyojifunua kwetu kwa njia mbali mbali , lakina hapa tutajifunza njia Nne.

1. MUNGU AMEJIFUNUA KATIKA NENO LAKE.

Ona jinsi alivyojifunua kwa Musa:-
(Kutoka 34:6)
"BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;"
(Zaburi 116:5)
"BWANA ni mwenye neema na haki,
Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema."

Maandiko yanasema kwamba Mungu ni mwenye huruma, fadhili, si mwepesi wa hasira ,mwenye neema, haki na rehema. Hivyo ndivyo Mungu wetu anataka tumfahamu.

(A) Nitaeleza kwanza neema rehema na haki.
Neema ni kupewa kitu chochote pasipo kustahili , unapewa bure tu bila sababu yoyote.Lakini hii ni tofauti na kupewa zawadi zawadi inaweza ikawa na sababu. Lakini Neema haina sababu.

Rehema ni kuhurumiwa, unahurumiwa katika jambo ambalo linataka likukabiri kama vile adhabu. Au unahurumiwa katika hali uliyonayo inayokusumbua kama vile shida ,umaskini magonjwa nk.

Haki ni kupewa kustahili . Haki maana yake unastahili kupata kitu fulani. Kwamfano unastahili kurithi , unastahili kulindwa. Unastahili hukumu . Tukisema huyu ni mtu wa haki maana yake anatenda kwa haki , yule anayestahili anampa kustahili kwake.

Mungu wetu amejifunua kwetu kwamba ni mwenye sifa hizo.Ona sasa jinsi anavyotutendea kwa sifa zake.:-

Sisi wakristo tumepewa NEEMA ya wokovu na kupewa HAKI ya kupata uzima wa milele . Tumepewa bure kabisa siyo juhudi zetu ,wala siyo kwa akiri zetu .
(Waefeso 2:8-9)
"Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu"

Tumeamini tu kazi ya msalaba wa Bwana Yesu aliyofanya .Tumekwisha kupewa NEEMA ya wokovu siyo tutapewa tumekwisha kupewa . Mkristo asiyejua NEEMA hii ya Mungu tuliyopata huyo mkristo anamwabudu Mungu asiyejulikana. Pia wapo wengine wanafikiri neema ya wokovu inapatikana kwa kumpendeza Mungu katika kushika Torati. Na wengine wanafikiri neema ya Wokovu inapatikana kwa kumpendeza Mungu katika kushika shera za kanisa. Na wengine hufikiri kwamba Mungu yupo sehemu amekaa akiwavizia watende makosa ili awape adhabu.

Lakini Mungu wetu amekwisha kutupa neema ya Wokovu ,sisi ni watoto wake . Sisi ni wana wa Mungu,tumezaliwa katika Roho wake na yeye mwenyewe tayari anakaa ndani yetu na sisi ndani yake kupitia Roho wake Mtakatifu.
(1 Yohana 3:1-2)
"Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.
Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo."

Kwahiyo Mungu wetu hatuvizii sisi ili tutende makosa ili atuhukumu au atupe laana ,ila anatusaidia sisi kuishi maisha yanayompendeza na kututumia katika kumtumikia kwa Roho Mtakatifu aliyepo ndani mwetu. Mungu wetu anatutakasa na uovu wote ,anatulinda anatusaidia kushinda majaribu ya yule mwovu anatuepusha na mipango ya Shetani yote. Haya yote kwasababu sisi ni watoto wake siyo kwasababu kuna vitu tumefanya . Ni neema yake iliyopo ndani ya kristo Yesu Bwana wetu.

Wapo wakristo wanasema Bwana Yesu anafanya hukumu ya upelelezi eti anawapeleleza kuwa wanashika sheria ya Bwana ,hawa watu wenye mafundisho haya wana mwabudu Mungu asiyejulikana .Bwana Yesu ni mwokozi ametuokoa na anaendelea kutuokoa na kutulinda, yeye ndiye anayetupa nguvu ya kushinda uovu ,yeye ndiye anaye tuepusha na mipango yote ya shetani.

Wokovu umekamilika tumeokolewa ,kama bado hujaokolewa Neema bado ipo Mgaukie Mungu akutoe katika mikono na utumwa wa shetani na kuwa mwanae.

Wapo watu wanafikiri kwamba wanatakiwa wafanye mambo mazuri ili Mungu akawape wokovu , Neema ya wokovu ni sasa siyo baada ya kufa. Kama unafikiri wokovu bado ujue unamwabudu Mungu asiyejulikana , lakini Mungu anayejulikana amekwisha jifunua kwetu kwamba ametoa Neema ya Wokovu.

Neema ya wokovu imetupa HAKI ya kuwa wana wa Mungu , kwa sababu sisi ni wana wa Mungu tumepata HAKI ya kuwa warithi wa Mungu ,pia kwa kuwa sisi ni wana wa Mungu tumepata HAKI ya kulindwa na Mungu ,HAKI ya kubarikiwa na Mungu , HAKI ya kusikilizwa na Mungu na HAKI ya kurithi uzima wa milele . Haya yote tumepata kwa NEEMA siyo kwa matendo.

Ukikuta mtu anakuambia toa sadaka ili Mungu akulinde au toa sadaka ili Mungu alinde mali zako , ujue huyo mtu anamwabudu Mungu asiyejulikana . Na ukikuta mtu anauza nguvu za Mungu kwenye makopo ya maji, au mtu anauza nguvu za Mungu kwenye shanga za kuvaa Ujue huyo Mtu anamwabudu Mungu asiyejulikana. Ukikuta mtu anakuambia toa sadaka ya utakaso ,au sadaka ya kuweka watoto wakfu , au mtu anakulazimisha kushika Torati kwamfano sabato au kutokula vyakula kama njia ya kwenda Mbinguni au kutoa sadaka kisheria kama mafungu ya kumi kama njia ya kuhesabiwa HAKI , ujue huyu mtu anamwabudu Mungu asiyejulikana.

Sisi wakristo tunamwabudu MUNGU ANAYEJULIKA. Mungu wetu amekwisha jifunua kwetu kwamba sisi ni watoto wake ,anatupa HAKI zote siyo kwa matendo ya sheria ila ni kwa Neema yake . Anatuvisha ,anatulisha, anatulinda ,anatupa amani ,anatupa upendo ,anatupa uzima wa milele na kurithi mambo ya Mbinguni kwa sababu sisi ni watoto wake siyo kwasababu tumetimiza sheria au siyo kwasababu tumetoa sadaka.

B. Mungu anasema Yeye ni Mungu Mtakatifu tena mwenye wivu.
(Kutoka 34:14)
"Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu"

Maana yake ni kwamba , Mungu wetu haabudiwi na miungu mingine wala sanamu. Mungu wetu hafananishwi na miungu mingine wala sanamu za aina yoyote. Kuna wakristo wanamwabudu Mungu na sanamu nyingine,sanamu zakushora na nyingine za kuchonga na nyingene za kuvaa na nyingine ni picha na wengine wanaabudu viongozi wao wa dini wanabeba picha za manabii wanatembea nazo, wanaweka picha za manabii na wachungaji wao kwenye nyumba zao . Lakini Mungu wetu anasema yeye ni Roho yupo kila sehemu na yupo ndani mwetu katika miili yetu . Kwanini tumwabudu kwa sanamu na picha na mishoro, kwanini tunatembea na picha za manabii na wachungaji ? Watu wanaofanya hivi wanamwabudu Mungu asiyejulikana.

Pia nimeona watu wanajiita walokole lakini ni wazinzi, washerati ,walevi ,wezi wamejaa chuki fitina wivu . Wanaonea wivu wa huduma ,wanagombania makanisa ,waongo ,wazushi wenye hila . Hawa nao wanamwabudu Mungu asiyejulikana .Mungu amejifunua hivi
(1 Petro 1:15-16)
"bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu"

Hivyo ndiyo Mungu wetu alivyojifunua kwetu , kama tukimwabudu tofauti na hivyo inamaana tunamwabudu mungu asiyejulikana.

2. MUNGU AMEJIFUNUA KWETU KWA NJIA YA MWANAE YESU KRISTO
(Yohana 1:1,14)
[1]Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
[14]Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli."
Yohana anatuambia hivi , hapo mwanzo kulikuwako Neno , Mwanzo haujulikani lakini huyu Neno alikuwepo na alikuwepo kwa Mungu na yeye Neno ni Mungu akaja kwetu na kufanyika mwili na kuishi na sisi . Yohana anasema wameona utukufu wa Mungu, neema na kweli ndani ya huyo Neno aliyefanyika mwili.

Kwa kumwona Bwana Yesu ,tumemwona Mungu Baba . Kila aliyemwona Bwana Yesu amemwona Mungu Baba
(Yohana 14:8-9)
"Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.
Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?"

Umeona aliyemwona Bwana Yesu amemwona Baba
Kila mwenye Bwana Yesu ana Mungu Baba. Kila aliyemkataa Bwana Yesu amemkataa Mungu Baba. Vile ambavyo Bwana Yesu ameishi na sisi ndivyo ambavyo Mungu Baba alivyo.
Bwana Yesu aliishi na sisi na anaishi na sisi kwa upendo Mkubwa, Bwana Yesu amejaa Rehema , Bwana Yesu amejaa Neema , Bwana Yesu amejaa Kweli na Haki. Hivyo ndivyo alivyo Mungu Baba. Bwana Yesu hakuwakimbia wenyeshida ,wala hakuwafukuza wenye dhambi, aliwatakasa wakoma ambao walikuwa wakitengwa kwa mujibu wa Torati. Alimtakasa mwanamke ambaye alikuwa anatokwa na damu ambaye kimsingi alikuwa ametengwa kwa mujibu wa Torati , Bwana Yesu alijitoa sadaka ya dhabihu ya dhambi kwa ajiri ya watu wote Duniani . Upendo huu na Rehema na Neema na unyenyekevu huu , ndivyo Mungu alivyo.

Usimkimbie Mungu ukiwa una dhambi ,unatakiwa umuendee Mungu ili akutakase , Mungu hakimbiwi Mungu ni mwenye upendo na Rehema .Umeona Bwana Yesu , watu walimkimbilia hawakumkimbia. Kuna watu wanaambiwa hiyo dhambi uliyofanya ni kubwa sana itabidi ufanye kazi kubwa sana ili Mungu akusamehe ,wanaambiwa itabidi ufunge sana ,utoe sadaka kubwa, ufanye vitubio vingi. Huu ni uongo Mungu hasamehe dhambi kwasababu mwadamu ametoa sadaka au kwasababu mwanadamu ameonyesha kujitesa . Mungu anasamehe dhambi kwa Rehema yake na Upendo wake.

Kila anayesema kwamba ana Mungu na ni Mtumishi wa Mungu lazima awe na upendo ,na Rehema .kama Mtu anasema ni mtumishi wa Mungu halafu hana sifa hizi , huyo mtu hana Mungu na hamjui Mungu . Mtu wa jinsi hii anamwabudu Mungu asiyejulikana.
Bwana Yesu alikuwa mnyenyekevu sana na mwenye upendo hata kufa msalabani kwa ajiri ya wenye dhambi. Aliweza kuteseka kwa ajiri ya wengine ,alijitoa kuwatumikia wengine na siyo kutumikiwa. Aliwafundisha wanafunzi wake kwamba anayetaka kuwa mkubwa awe mtumishi wa wengine. Hakutaka viongozi wa wakristo kujiinua na kujitukuza na kunyenyekewa kupita kiasi hata kufika mahali pakutaka kuabudiwa .

(Mathayo 20:26-28)
"Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;
na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;
kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi"

Je unafikiri sasa hivi iko hivyo makanisani? Kwamba yule aliyemkubwa ni mtumishi wa watu. Je anawatumikia watu au anatumikiwa? Makanisa sasa hivi yanafanya kazi ya kuwatumikia viongozi wao. Viongozi huweka sheria na tamaduni nyingi za kuhakikisha wanatumikiwa na kunyenyekewa kama miungu, wanawalazimisha watu kuwaita Baba siyo kwasababu wanataka heshima ila kwasababu wanataka kutumikiwa ,kutukuzwa na kuabudiwa. Wakristo mwaka mzima wanahangaika jinsi ya kumwinua kiongozi wao kimaisha. Watu wanamna hii wanamwabudu Mungu asiyejulikana. Bwana Yesu anataka tufanane naye .


3.MUNGU AMEJIFUNUA KWETU KWA NJIA YA ROHO WAKE ANAYEKAA NDANI MWETU.
(Ezekieli 36:26-27)
"Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.
Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda."

Hii ahadi ya Baba yakutuzaa kwa Roho Mtakatifu ilitimia na inatimia kwa kila anayemwamini Bwana Yesu . Roho Mtakatifu ni Roho ya Mungu, ni Mungu mwenyewe, hivyo basi tunaweza kumfahamu Mungu kupitia Roho wake , maana Roho wake hutufunulia jinsi Mungu alivyo kwasababu Roho Mtakatifu yupo ndani ya Mungu na yupo ndani mwetu.

(1 Wakorintho 2:11)
"[11]Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.
Tunayafahamu mambo ya Mungu kwa Roho Mtakatifu na tunamfahamu Mungu kwa Roho Mtakatifu. Ukikuta mtu anapinga utendaji wa Roho Mtakatifu ndani ya wakristo huyu anamwabudu Mungu asiyejulikana.

(Waebrania 8:10-11)
[10]Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli
Baada ya siku zile, asema Bwana;
Nitawapa sheria zangu katika nia zao,
Na katika mioyo yao nitaziandika;
Nami nitakuwa Mungu kwao,
Nao watakuwa watu wangu.
[11]Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake,
Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana;
Kwa maana wote watanijua,
Tangu mdogo wao hata mkubwa wao."

Roho Mtakatifu anatufunulia kila kitu ,ndiye anatufundisha kweli yote ,yaa Neno la Mungu . Ndiye anaihuisha miili yetu. Yaani ile hali ya kutupinga na kututia katika dhambi inapungua ,hatimaye tunaweza kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu.Roho Mtakatifu haingii ndani ya mtu kukaa tu , anaingia kutenda kazi na utendaji wake unaonekana .
Utendaji wake unaonekana katika karama za Roho na Matunda ya Roho Mtakatifu. Kuna watu hawajui kwamba matunda ya Roho Mtakatifu pia ni udhihirisho wa Mungu.Matunda ya Roho Mtakatifu yakionekana ndani mwako maana yake wewe una Mungu ndani mwako.
(Wagalatia 5:22-23)
[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
[23]upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria"

Roho Mtakatifu anamuumba mtu ,Mtu anapata badiliko la kutoka ndani, ili aishi katika ule utakatifu ambao Mungu anapenda.Mtu anakuwa na upendo ,upendo unaotoka ndani siyo ule wa nje wa sheria ambao ni wakinafiki ,huu ni upendo wakutoka ndani. Tunakuwa na furaha ,amani ,uvumilivu,utu wema ,fadhili ,uaminifu ,upole,kiasi vyote hivi ni vyakutokea ndani ya mtu , vikitokea nje vinakuwa ni vyakinafiki ndiyo maana katika hivyo hakuna sheria , maana sheria haiwezi kusimamia utu wema au fadhili au uaminifu.

Hivyo ndivyo Mungu alivyojifunua kwetu kwa kipindi hiki cha Neema ,ikiwa mtu leo atafundisha sheria za nje kama za Torati huyu anamwabudu Mungu Asiyejulikana.
Roho Mtakatifu anatupa karama , lakini wapo wanapinga karama hizo na wengine kuzitukana . Wakristo kama hawa wanamwabudu Mungu asiyejulikana.

4. MUNGU AMEJIFUNUA KATIKA NGUVU ZAKE.

Tunamjua Mungu pia katika utendaji wa Nguvu zake. Mungu wetu siyo katika andiko tu , nikatika Neno na Nguvu za utendaji.

(2 Petro 1:16)
"Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake."

Maana yake Injili siyo hadithi, Ni ukweli ambao unajidhihirisha katika nguvu za Mungu. Mungu anaonekana kwanza kwa rehema na neema anayoiashiria kwa watu hadi wanafikia kutubu hadi kuzaliwa kuwa wana wa Mungu kwa Roho wa Mungu. Hiyo ni nguvu ya Mungu.

(1 Wakorintho 4:19-20)
"Lakini nitakuja kwenu upesi, nikijaliwa, nami nitafahamu, si neno lao tu waliojivuna, bali nguvu zao.Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu".

Umeona Mungu wetu amejifunua katika nguvu kwa watu wake. Roho Mtakatifu anayekaa ndani mwetu anadhihirika katika nguvu
Nguvu za Mungu zinaonekana kwa watu wake . Zinakaa ndani ya watu wake, zinaonekana katika utendaji.
Watu wengi hufikiri kwamba nguvu za Mungu ni miujiza tu, au uponyaji au kufufua wafu . Hawajui kwamba nguvu za Mungu kwanza kabisa ni katika neema ya wokovu na kudhihirika kwa tunda la Roho Mtakatifu ndani ya mtu. Na ndiyo maana manabii wengi wa uongo wanaficha maisha yao kwasababu hawataki watu wajue kwamba hawana tunda la Roho Mtakatifu. Shetani ataigiza nguvu za Mungu na miujiza mingi lakini hawezi kuwa na Matunda kama yale anayotoa Roho Mtakatifu, Ndiyo maana Bwana Yesu akasema mtawatambua kwa Matunda yao.
(Wagalatia 5:22-23)
"Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria"
Sasa unakuta mtu anatenda kweli miujiza lakini hana upendo. Anajisifia nguvu lakini hizo nguvu siyo za Mungu wetu , ni za mungu asiyejulikana.
Tunalindwa na nguvu za Mungu
(1 Petro 1:5)
"Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho"
Umeona tunalindwa na nguvu za Mungu. Nguvu za Mungu zipo kila sehemu ni kama Roho ya Mungu . Huwezi kubeba nguvu za Mungu kwenye kitu cha kuvaa . Nguvu za Mungu siyo hirizi ,Nguvu za Mungu siyo mafuta ya upako wala maji ya upako wala sabuni za upako. tunalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani iliyopo katika kristo Yesu Bwana wetu. Ukikuta watu wanauziwa vitu venye upako na kusema uvae hivi vina Nguvu ya Mungu hao watu wanamwabudu mungu asiyejulikana.

Mungu akubariki


Na.Mwl Godlisten. w. Mshigheni
Www.vop.info.tz
0789874316