Moja ya andiko linalo wasumbua baadhi ya wakristo ni hili hapa ambalo amesema Bwana Yesu :- (Mathayo 23:9)
"Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni"

Watu huuliza Biblia inakataza kumwita mtu Baba Duniani inakuwaje tunawaita wachungaji Baba ?
Na wengine wanapenda sana kuitwa Baba ,kwanini?

Ili tuweze kulijibu swali hili lazima kwanza tuangalie muktadha wa katazo hili la Bwana Yesu. Je Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema msimwite mtu Baba duniani?

(Mathayo 23:1-12)
"[1]Kisha Yesu akawaambia makutano na wanafunzi wake, akasema,
[2]Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa;
[3]basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.
[4]Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.
[5]Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao;
[6]hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi,
[7]na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
[8]Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.
[9]Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.
[10]Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.
[11]Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.
[12]Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa"

Sasa umeona ukisoma kwa umakini maandiko hayo ya Mathayo utagundua Bwana Yesu alichokataza . Aliwatazama mafarisayo na waandishi jinsi walivyokuwa wanaishi ukayaona haya:-
1.Walikuwa ni watu waliokuwa wanapenda sana kunyenyekewa isivyokawaida.
2. Walikuwa wanapenda sana kuonekana ni watakatifu kuliko wengine.
3.Walikuwa wanapenda kuwashurutisha watu wafanye mambo ambayo wao wenyewe hawawezi kuyafanya.
4.Walikuwa wanapenda kutukuzwa na kuabudiwa.
5.Walikuwa wanajiona kwamba wao wako na Mungu kuliko wengine.

Kwanini walikuwa wanayapenda haya ? Kwasababu walikuwa na elimu kubwa ya Dini na wana mamlaka ndiyo maana wanaitwa Rabi ( Mwalimu) ,Viongozi na Mababa.

Bwana Yesu hakupenda kanisa liwe na tabia hizi za mafarisayo na Waandishi, kimsingi Bwana Yesu hakukataza watu kuitwa walimu wala viongozi ndiyo maana hata leo uwalimu ni karama ya Roho Mtakatifu na Uongozi pia ni karama ya Roho Mtakatifu kama ni hivyo basi Roho Mtakatifu asingetoa karama hizo.

Kwahiyo kimsingi Bwana Yesu alikataza matumizi mabaya ya maneno haya yaani Baba , (Rabi)Mwalimu na kiongozi.

Kwa bahati mbaya sana , KANISA LA LEO linatumia neno BABA VIBAYA , wengi hutumia neno Baba kama vile mafarisayo na waandishi walivyokuwa wakilitumia na tabia zao.
Leo tunaona watu wanalazimishana kuitana Baba , mchungaji analazimisha watu wamwite Baba, asipoitwa Baba anaona hanyenyekewi, haogopwi hatukuzwi , haya ndiyo aliyokataza Bwana Yesu matumizi mabaya ya neno Baba.

Mbaya zaidi Kanisa la leo limetengeneza IMANI POTOFU KUHUSU NENO BABA . Ili tuweze kueleza jambo hili lazima tujifunze kwanza maana ya neno Baba katika Biblia .
1. Maana ya kwanza ya neno Baba katika Biblia ni baba aliyetuzaa katika mwili .
(Matendo ya Mitume 13:32)
"Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa,"

2. Maana ya pili ya Neno Baba katika Biblia ni mwanzilishi wa kitu kwa mtu kama imani au mwazishi wa kitu katika jamii.
(1 Wakorintho 4:15)
"Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili".

3. Maana ya tatu kubwa kuliko zote ni Mungu ( Yaani Baba aliyetuumba na aliyetuzaa katika Roho Mtakatifu na mwanzilishi wa kila kitu).
(Waebrania 12:9)
[9]Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya BABA WA ROHO ZETU na kuishi?

Sasa matumizi ya neno Baba ya kwanza yaani Baba aliyetuzaa katika mwili hua matumizi haya hayana utata katika jamii yetu . Kila mtu humwita mtu aliyemzaa katika mwili Baba bila shida yoyote, tena ni jambo sahihi kwa Mujibu wa Neno la Mungu.

Matumizi ya pili na ya tatu ndiyo huleta utata kwa wakristo wengi . Kwamfano huchanganya Baba kama mwanzilishi wa kitu na Baba wa kiroho.
Baba mwazilishi wa kitu akiwa yeye amemwazishia imani anamwita Baba wa kiroho badala baba mwazilishi wa Imani.
Baba wa kiroho ni mmoja tu naye ni Mungu wetu tu.
Hatuna Baba wa kiroho mwanadamu. Najua utashangaa kwasababu wengi huitana Baba wa kiroho na mama wakiroho. Lakini ni ukweli tena niukweli kabisa kwamba hakuna maana hii kwenye Biblia kwamba mtu anaweza kuwa baba wa kiroho wa mtu mwingine
Baba wa kiroho maana yake amekuumba na amekuzaa katika roho , je mwanadamu anaweza kumzaa mtu katika Roho. Je mwanadamu anaweza kumjaza mtu Roho ? Kama jibu siyo kwanini tumwite mtu Baba wa kiroho. ?

Mtu anayekufundisha neno la Mungu na ukakua katika imani huyo ni Baba anayesimamia imani yako siyo vibaya ukimwita Baba lakini siyo Baba wa kiroho.
Mtu aliyekuhubiria injili na ukaokoka ni Baba aliyeanzisha imani ndani mwako siyo vibaya ukimwita Baba .Lakini siyo baba aliyekuzaa katika Roho. Mungu pekee ndiye aliyetuumba na anayetuzaa katika Roho.

(Yohana 3:3-6)
[3]Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
[4]Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
[5]Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
[6]Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho"

Kutokana na upotoshaji huu watu wengi wametengeza imani potufu juu ya neno Baba.

1. Wapo wakristo wanaamini kwamba ili Mungu akubariki lazima Baraka zako zipitie kwa Baba wa kiroho, Wakiamini kwamba Baba wa kiroho amekushirikisha Roho yake.
2. Wengine wameaminishwa kwamba ili useme na Mungu au Mungu aseme na wewe lazima Baba wa kiroho awe Muunganishi.
3.Kwa upotoshaji huu wengine wanaamini kwamba Baba wa kiroho amekuwa sana kiroho kuliko yeye.
4. Wengine wameaminishwa kwamba huwezi kumpita Baba wa kiroho katika kuyafahamu mambo ya Mungu.
5. Wengine wameaminishwa kwamba huwezi kumkemea Baba wa kiroho pale anapokosea.

Hizi imani potofu zimeletwa na Shetani ili wakristo wafungwe katika vifungo vya watumishi wa uongo. Watumishi wa Uongo hulifanya kanisa kuwatumikia wao badala ya wao kulitumikia kanisa . Watumishi wa Uongo wao hupenda sana kunyenyekewa ila wenyewe hawataki kunyenyekea. Watumishi wa Uongo hupenda kupewa kuliko kutoa . Watumishi wa Uongo hupenda kutengeza mafundishi ya kuwagandamiza watu na kuwanyonya huku wakimsingizia Mungu. Haya ndiyo Bwana Yesu aliyoyaonya Hakutaka kanisa liwe hivi , ona hapa:-

(Mathayo 20:25-28)
[25]Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.
[26]Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;
[27]na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;
[28]kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi."

Sasa ona Bwana Yesu anavyosema, je nikweli kwamba wale wanaotaka kuitwa Baba leo hii wanayazingatia hayo maneno ya Bwana Yesu? Huoni kwamba wale wanao lazimisha leo hii kuitwa Baba ni wale wenye tabia za mafarisayo na waandishi . Siyo wale wanaojitoa kwa ajiri ya wengine siyo wale wanaojinyenyekeza kama Bwana Yesu alivyonyenyekea siyo wale wanaotaka kuwa watumwa ila ni wale wanaotaka kuwa mabwana.

Kumwita mtu Baba siyo dhambi ndiyo maana hata wale waliotuzaa katika mwili tunawaita Baba . Swala ni kwamba unamwita baba ukimaanisha nini ? Na yeye anayepokea hilo neno Baba anamaanisha nini na analitumiaje au anataka nini ?
Kanisa la kwanza lilitumia neno Baba na mwana kwa mfano:-

(1 Timotheo 1:18)
[18]Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita vizuri"
Umeona mtume Paulo anamwita Timotheo mwanangu kwa maana yeye ni Baba.

(3 Yohana 1:4)
"Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli"
Mtume Yohana anawaita wakristo hao wanangu kwa maana yeye ni Baba.

(1 Wakorintho 4:15-16)
"Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.Basi, nawasihi mnifuate mimi."

Umeona mtume Paulo anavyosema anasema mna walimu wengi KATIKA KRISTO ila yeye amewazaa KATIKA KRISTO KWA NJIA YA INJILI. Hao walimu wanafundisha mafundisho ya Bwana Yesu ila yeye Mtume Paulo ndiye mwazilishi wa IMANI YA UKRISTO ndani ya hao watu . Kwahiyo Mtume Paulo hajawazaa hawa KATIKA ROHO . wala hajajiita Baba wa Kiroho wala hajasema nimewazaa katika Roho. Yeye ni Baba aliyeanzisha imani ya ukristo ndani mwao.
Sasa kuna watu wanapotosha hapa wanasema Baba wa roho ,hajajiita baba wa Kiroho wala hajasema amewazaa katika Roho.

Angalia Biblia inavyosema juu ya Baba wa roho zetu:-
(Waebrania 12:5-9)
[5]tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana,
Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana,
Wala usizimie moyo ukikemewa naye;
[6]Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi,
Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
[7]Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?
[8]Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.
[9]Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya BABA WA ROHO ZETU NA KUISHI?

Baba wa roho zetu aliyetajwa hapo ni Mungu siyo mwanadamu.Kuna watu wananyofoa huo mstari mmoja wa 9 nakupotosha na kuwafundisha watu kwamba Baba wa roho zetu ni mchugaji. Mwanadamu kujiita Baba wa roho ni makosa makubwa . Hatuoni sehemu yoyote katika Biblia inayosema mwazilishi wa Imani ndani ya mtu ni Baba wa kiroho au ni Baba wa roho zetu au ametuzaa katika roho. Kusema Baba wa kiroho au mama wa kiroho ni mapokeo ya wazee tu ni mafundisho ya dini tu hayana msingi katika neno la Mungu . Sasa shida ni kwamba neno hili Baba wa kiroho na mama wa kiroho limezua mafundisho ya uongo kama nilivyoeleza mwanzo na limerudisha tabia za mafarisayo na waandishi katika kanisa kama vile Bwana Yesu alivyokataza.

Kama unamwita mshungaji wako Baba mwite ukimaanisha kwamba ni mwazilishi wa imani ya ukristo ndani mwako au umwite kwa heshima tu ila si vinginevyo. Na hii isikuzuiye kumkemea au kumwonya pale anapokosea . Na hii haina maana kwamba yeye yuko karibu na Mungu kuliko wewe . Tena haina maana kwamba yeye anayafahamu mambo ya Mungu kuliko wewe. Na hii isimfanye kwamba asiwe mnyenyekevu kwako.

Kama kanisa likiaminishwa kwamba huyu ni Baba Mtakatifu ,siku huyo Baba Mtakatifu akikosea mtawezaje kumkemea? Mtu akiaminishwa kwamba mimi nimekuzaa katika roho na wewe ni mwanangu wa kiroho , baraka na laana zako zinatokea kwangu, siku huyu Baba wa kiroho akikosea atawezaje kumkemea ?

Neno hili Baba wa Kiroho limezua mafundisho mengi ya uongo . Imefika mahali watu wanatembea na picha za Baba wa kiroho kwenye mifuko na wengine wamebandika kwanye kuta za nyumbani zao , na wengine kwa imani kwamba Baba wa kiroho anaweza kukuletea laana au baraka basi wamekuwa waoga hata pale Baba wa wakiroho anapokosea hawamkosoi. Wengine kwa kuaminishwa kwamba ili useme na Mungu au Mungu aseme na wewe lazima Baba wa kiroho awe kiunganishi hivyo wamefanywa watumwa wa mafundisho ya uongo na kusikiliza Mashetani.

Sisi wa Wakristo Baba yetu wa Kiroho au Baba wa roho zetu ni mmoja naye ni Mungu ndiye Baba yetu na Mungu wetu na mwazilishi wa kila jambo. Kama unamwita Mchungaji wako Baba mwite kwa HASHIMA TU kwamba anasimamia imani yako au ni mwazilishi wa imani yako ndani yako lakini siyo vinginevyo.


Na. Mwl.Godlisten Mshigheni
Www.vop.info.tz
0789874316