(Zaburi 105:4)
"Mtakeni BWANA na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote."

(1 Wakorintho 4:19-20)
"Lakini nitakuja kwenu upesi, nikijaliwa, nami nitafahamu, si neno lao tu waliojivuna, bali nguvu zao.
Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu"

Nguvu za Mungu ni kudhihirika kwa utendaji wa Mungu. Utendaji wa Mungu unadhihirika pale Mungu akiwa ndani mwetu. Kwa kuwa Mungu anakaa ndani mwetu na sisi ni Hekalu la Mungu tutaziona nguvu zake ndani mwetu na katika maisha yetu na katika huduma.

Walitokea walimu wa uongo katika kanisa la wakorintho wakifundisha watu Injili ya uongo , Mtume Paulo akasema nitakuja kulifahamu neno lao wanalofundisha ,siyo neno tu pamoja na nguvu zao. Kwanini alisema hivi?

Kwasababu nguvu za Mungu zinaambata na Neno la kweli la Mungu .Na Neno la kweli la Mungu linaambatana na Nguvu za Mungu.

Kama watu wanafundisha uongo katika kanisa ,nguvu za Mungu haziwezi kuonekana .maana Mungu ni Mungu wa KWELI , na Nguvu zake zinadhihirika katika KWELI TU.

Kimsingi mtu yoyote mwenye Roho Mtakatifu ana nguvu za Mungu, Roho Mtakatifu ni Mungu anapokuwa ndani mwetu utendaji wake unaonekana . Roho Mtakatifu haingii ndani ya mtu ili akae tu . Akiingia ndani ya mtu anambadilisha ,anamfundisha anamfanya mtu atende mapenzi ya Mungu. Roho Mtakatifu akiwa ndani ya mtu tunda la Roho Mtakatifu linaoneka na karama zake zinaonekana, kudhihirika kwa matunda ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu na karama ni kudhihirika kwa Nguvu za Mungu ndani ya mtu. Watu wenye Roho Mtakatifu ndiyo walio ndani ya Ufalme wa Mungu, ndiyo wenye nguvu za Mungu.(Mathayo 11:12)
"Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka".

Kwahiyo nguvu za Mungu siyo kutenda miujiza tu na kuponya watu na kutabiri mafanikio kwa watu tu ,kama wakristo wengi wanavyojua. Nguvu za Mungu ni zaidi ya hayo. Nguvu za Mungu ni pamoja na kudhihirika kwa tunda la Roho Mtakatifu ndani ya Mtu.
(Wagalatia 5:22-23)
"Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria."

Ni rahisi sana watu kuona kwamba mtu anayetenda miujiza ana nguvu za Mungu kuliko kuona kwamba mtu mwenye upendo ana nguvu za Mungu. Ndiyo maana Shetani ana wadanganya na kuwaletea watumishi wa uongo, wenye nguvu zake za kutenda miujiza na ishara nyingi na mafundisho ya mashetani. Lakini watumishi hao ukiyatazama maisha yao hawana tunda la Roho Mtakatifu. Wala hawafundishi Neno la Mungu kwa ufasaha, wala hawana nia ya kuponya roho za watu ila wanania na vitu vya mwilini tu. Ndiyo maana Bwana Yesu anasema mtawatambua kwa matunda yao.

Kwanini wanakuwa hivyo ? kwa sababu wakristo wengi nao wanapenda kuponya miili na kushibisha miili kuliko roho. Wakristo wanahangaika na vitu vinavyo haribika kuliko visivyoharibika.
(Yohana 6:26-27)
"Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu."

Shetani anajua watu wanapenda chakula chenye kuharibika .kwahiyo ndiyo maana anaweka watumishi wake wengi wanazungumza mambo ya Dunia tu na kunia mambo ya Dunia na kudhihirisha nguvu za uongo.
(Wafilipi 3:19)
"mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani"

Shetani anajua watu wanapenda nguvu ziwatendee kazi ila Mungu hawamtaki . Kwanini na sema hivi ? Kwasababu mtu anapenda kuombewa apone , anataka aone muujiza wa Mungu katika maisha yake anataka aone nguvu za Mungu zikifanya kazi katika kazi yake, biashara yake lakini hayuko tayari kutubu na kumpokea Bwana Yesu kama Bwana na Mwokozi wake . Kwakuwa watu wana kiu na nguvu za Mungu ila hawana kiu na Mungu hii imesababisha kuzuka kwa mafundisho Mengi ya uongo kuhusu nguvu za Mungu.

Mafundisho hayo ni kama :-

1. Kuuza nguvu za Mungu
Wapo watumishi hutengeneza vitu ambavyo wanadai wanavitia nguvu za Mungu ( maalufu kama upako) na kuviuza , wakristo hununua vitu hivyo wakiaminishwa kwamba vina nguvu ya Mungu , vingine ni vya kuvaa kama shanga, vingine vya kuweka ndani ya nyumba ,vingine vya kupaka na vingine vya kunywa . Vitu hivi huuzwa bei tofauti tofauti kulingana na ukubwa au ukubwa wa nguvu wanazoaminishwa kwamba zipo humo ndani. Wakristo wengi kwa kukosa maarifa hununua na kuamini vitu hivyo. Wakristo wamekuwa kama vile washirikina wanavyotegemea hirizi au sanamu. Wakristo wamerudishwa katika kuabudu sanamu bila wao kujitambua kwamba wanaabudu sanamu.

Wakristo tunamwabudu Mungu katika Roho na Kweli ,Mungu wetu anakaa ndani mwetu
(Yohana 14:17)
"ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu"

Mungu yupo ndani mwetu kupitia Roho wake Mtakatifu na uweza na nguvu zake zinadhihirika akiwa ndani mwetu.

Mungu wetu hauzwi ,nguvu za Mungu ni Mungu mwenyewe .Mtu akikudanganya kwamba nunua mafuta ya upako au maji ya upako au nguo za upako au mikufu ya upako ,huyo ni mwongo maana nguvu za Mungu ni Mungu mwenyewe huwezi kumbeba Mungu kwenye chombo. Ukiwa na Mungu wako ndani mwako , Nguvu zake zinaonekana katika maisha yako.
Mungu anatutendea kwa neema yake.

2. Kutafuta Nguvu za Mungu kwa sadaka.

Haya pia ni mafundisho potofu juu ya nguvu za Mungu. Mtu anataka nguvu za Mungu zimtendee lakini anapotoshwa jinsi ya kuzipata. Atapewa masharti mengi ya sadaka na kufundishwa imani potofu. Utasikia toa sadaka ya kuzindika nyumba yako,Toa sadaka ya kukomboa gari,Toa sadaka ya kukomboa shamba ,panda mbengu ya kuanzisha bishara. Haya yote ni mafundisho potofu juu ya nguvu za Mungu. Nguvu za Mungu hazipatikani kwa sadaka . Sadaka pekee ya kutumia kuongea na Mungu na kumsihi Mungu ili atutendee ni sadaka ya Bwana Yesu. Sadaka ya damu ya Bwana Yesu iliyomwagika msalabani ndiyo tuliyopewa ndiyo hiyo pekee inayotupa kibali cha kusema na Mungu na Mungu akatenda . Siyo sadaka za ng'ombe ,Mbuzi na pesa. Karama ya Mungu ( zawadi ya Mungu) haipatikani kwa mali inapatikana kwa Neema .
(Matendo ya Mitume 8:18-20)
"Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemwekea mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali."

Nataka uone hapo jinsi Mtume Paulo anavyomkemea simoni kwamba karama ya Mungu haipatikani kwa mali. Karama maana yake ni zawadi kutoka kwa Mungu , kwa mfano anayepokea uponyaji anapewa zawadi na Mungu na anayeombea mtu akapona pia amepewa zawadi kutoka kwa Mungu. Huo ni utendaji wa nguvu za Mungu haupatikani kwa pesa unapatikana kwa Neema ya Mungu mwenyewe.

VIKWAZO VINAVYOZUIA KUPATA NGUVU ZA MUNGU.

1. Kuabudu kwa mizaha.

Kama watu wanaishi na kumwabudu Mungu kwa mizaha Nguvu za Mungu haziwezi kuonekana . Kwakuwa Mungu hapendi mizaha. Leo unatubu kesho uko kwenye uzinzi , leo unatubu kesho unaiba hiyo ni mizaha, unatamani kumtumikia Mungu lakini pia umejaa tamaa za mambo ya Dunia hiyo ni mizaha . Unamsifu Mungu na nyimbo nzuri lakini nyimbo za Dunia zote unazijua hiyo ni mizaha . Unamtumikia Mungu ili upate pesa vyeo na mali hiyo ni mizaha.

Sasa mizaha hii imefanya wakristo wengu kukosa nguvu za Mungu , wanamwabudu Mungu katika mfumo wa kidini tu . Mungu hataki mizaha anasema:-
(Zaburi 1:1-2)
"Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku."

Ukiamua kusimama na Mungu katika maisha yako uwe na msimamo maana Mungu hapendi watu wanaoyumba katika imani.
(Luka 9:62)
"Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu."
Imani yako isiwe na michanganyo changanyo.(Waebrania 10:38)
"Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani;
Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye"
Kusita sita ndiyo huko kuabudu kwa mizaha. Ukiabudu kwa mizaha hutaziona nguvu za Mungu zikikutendea kazi.

2. MAFUNDISHO YA UONGO.
Mafundisho ya uongo yanatengeneza imani potofu .Makanisa yanayofundisha imani potofu si rahisi Nguvu za Mungu kuonekana zikitenda kazi. Kama watu wafundishwa kuomba watakatifu waliokufa ,hapo Nguvu za Mungu zitapatikana vipi? Unakuta mtu kila siku anaomba wanadamu wenzake waliokufa ,eti kwasababu walikuwa ni watakatifu halafu anategemea nguvu za Mungu ,hapo Nguvu za Mungu haziwezi kutokea.

Yapo makanisa yanamkufuru Roho Mtakatifu , mengine yanasema Roho Mtakatifu ni Nguvu siyo Mungu. Na wengine wakiona karama za Roho Mtakatifu kama kunena kwa Lugha wanasema ni Mapepo . Sasa makanisa kama haya hayawezi kupata Nguvu za Mungu.


Www.vop.info.tz